Na Mwandishi wetu- Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, ameipongeza Taasisi ya tiba ya mifupa na ubongo Muhimbili (MOI) kwa kuzijengea uwezo hospitali za mikoa ikiwemo Mwananyamala, Tumbi, Temeke, Amana na Morogoro kuwahudumia wagonjwa wa dharura za ajali na kiharusi.
Dkt. Shekalaghe ametoa pongezi hizo leo octoba 17, 2025 wakati akifunga mafunzo hayo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, iliyowahusisha Madaktari bingwa na bobezi kutoka MOI, hospitali ya Benjamin Mkapa na Wauguzi wabobezi wa MOI wa huduma za kiuguzi kwa wagonjwa waliopata majeraha kwenye Ubongo , uti wa mgongo na mishipa ya fahamu.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupunguza rufaa nyingi zisizo za lazima kwenda hospitali za mbali kwa kuimarisha huduma za dharura za upasuaji wa mishipa ya fahamu, mgongo, ajali za mifupa na huduma za wagonjwa mahututi (ICU)
Dkt. Shekalaghe amesema katika kipindi kifupi cha mafunzo hayo jumla ya rufaa za wagonjwa 67 ambao walipaswa kwenda MOI hazikutolewa kutokana na wagonjwa hao kunufaika na mafunzo ambayo yametolewa kwa kipindi cha mwezi mmoja na wataalam wa hospitali hizo.
“Leo napenda kutoa pongezi za dhati na shukrani kwa Mkurugenzi wa MOI Dkt. Mpoki Ulisubisya kwa kutekeleza maelekezo yangu kwa ufasaha mkubwa ambapo leo timu ya MOI inahitimisha mafunzo ya awamu ya kwanza ya kuzijengea uwezo hospitali za rufaa za mikoa kuhudumia wagonjwa wa dharura za ajali na kiharusi” amesema Dkt. Shekalaghe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ameshukuru kwa pongezi hizo na kusema kuwa Taasisi ya MOI itaendelea kuzijengea uwezo hospitali zingine za mikoa nchini Tanzania kwani Serikali imefaya uwekezaji mkubwa kwa wataalam na vifaa tiba.