Dkt. Mpoki apongeza huduma bora za kibingwa za MOI sabasaba

Na Abdallah Nassoro-Sabasaba

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya leo Julai, 4, 2025 ametembelea banda la kutolea huduma la taasisi hiyo katika maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mpoki ambaye alipokelewa na mwenyeji wake Meneja Uhusiano wa MOI Bw. Patrick Mvungi ameelezea kufurahishwa kwake na namna watumishi katika banda hilo wanatoa huduma bora za kibingwa na kibobezi kwa wagonjwa pamoja na elimu kwa wananchi.

“Nawapongezeni sana kwa kazi nzuri munayoifanya, endeleeni kuwahudumia Watanzania kwa moyo huohuo wa upendo na ukarimu…tumeamua kusogeza huduma hizi za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu hapa Sabasaba ili wananchi wengi waweze kufaidika nazo” amesema Dkt. Mpoki

Awali Meneja Uhusiano Bw. Mvungi alimweleza mkurugenzi mtendaji huyo kuwa, MOI inatoa huduma kwa gharama nafuu katika maonesho hayo ili kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kupata huduma za kibingwa

“Kwa wale wenye kadi za bima ya afya wanapokelewa na kupatiwa matibabu kwa mfumo huo na wale ambao hawana bima wanalipia kiasi cha Tsh.5,000 kumuona daktari bingwa…hizi ni gharama nafuu sana kwetu” amesema Mvungi

Katika hatua nyingine Dkt. Mpoki ametembelea mabanda ya hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Kansa ya Ocean road na kupongeza huduma bora wanazotoa kwa wananchi.

Katika maonesho hayo MOI inatoa huduma za kliniki kwa watu wenye matatizo ya mifupa, nyonga, goti, mgongo, ubongo, mishipa ya fahamu, fiziotherapia na upimaji wa ultrasound.

About the Author

You may also like these