Na Amani Nsello- JKCI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ameagwa na watumishi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) huku akiwasihi watumishi wa Taasisi hiyo kuzingatia miongozo ya utendaji wa kazi (SOP’s).
Hafla hiyo imefanyika leo Jumatano Januari 15, 2025 baada ya kuhudumu katika taasisi hiyo kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kama daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi kabla ya Desemba 2, 2024 alipoteuliwa na Mhe: Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtednaji wa MOI.
Dkt. Mpoki amesema kuwa ni muhimu kwa watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo ya kiutendaji (SOP’s) ili kuendelea kulinda maadili na kuboresha utoaji huduma sehemu za kazi.
“Ni muhimu kufuata miongozo ya utendaji kazi (SOP’s) wakati wa kutekeleza majukumu yenu, muwe na utaratibu maalum wa kufanya kazi, msiyumbishwe au kufuata utaratibu tofauti na miongozo na kanuni inavyotaka, mnapokea wageni hapa wanaokuja kujifunza kazi (Internship) muwaelekeze kanuni na miongozo yenu”- amesema Dkt. Mpoki
Aidha, Dkt. Mpoki amewashukuru watumishi wa JKCI kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi chote alichokuwa akifanya kazi katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge amewaomba watumishi wa taasisi hiyo kuiga mfano wa Dkt. Mpoki wa kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuwahi kazini.
“Licha ya cheo chake (Ubalozi) Dkt. Mpoki alikuwa akiwahi sana kazini, yaani nilikuwa nikifika hapa kazini (JKCI) saa 1 asubuhi nakuta gari yake imepaki, najiuliza huyu mtu anakuja saa ngapi?… Lakini pia alikuwa akifanya kazi kwa weledi na bidii mno, hivyo nawaomba watumishi wenzangu muige mfano wa Dkt. Mpoki” amesema Dkt. Kisenge