Na Abdallah Nassoro- MOI
Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imefanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika taasisi hiyo ambapo imewapongeza wafanyakazi kwa kutoa huduma bora wa wagonjwa.
Ziara hiyo ya siku mbili imeanza leo Septemba, 03, 2025 ambapo wajumbe wa bodi hiyo walikagua maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ikiwa pamoja na sehemu ya kuhifadhia dawa, radiolojia, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (New OPD), huduma za wagonjwa maalumna wakimataifa na fiziotherapia.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Augustino Mbogella amesema bodi ya wadhamini imeridhishwa na hali ya utoaji huduma katika taasisi hiyo na inawapongeza watumishi kwa kutoa huduma kwa weledi.
“Kwanza kabisa niwapongeze wafanyakazi wote kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwahudmia watanzania wenzetu wenye changamoto, endeleeni aro hiyo…tumefurahishwa na hali ya usafi, kila tulipopita tumeona mazingira ni masafi, hongereni sana” amesema Bw. Mbogella
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amewaeleza wajumbe wa bodi hiyo kuwa licha ya mafanikio makubwa ya kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa na ubongo kwa wananchi, menejimenti imedhamiria kupanua maneo ya kutolea huduma ili kupunguza msongamano wa wagonjwa wa nje.
“Kukamilika kwa ujenzi huu wa jengo la wagonjwa wa nje (New OPD) kutapunguza msongamano wa wagonjwa uliopo kwa sasa, lakini pia mradi wa iliyokuwa hospitali ya Tumaini (X-Tumaini) utawezesha kupanuka kwa huduma za MOI badala ya wote kuja kupata huduma eneo moja” amesema Dkt. Mpoki
Kikao cha bodi ya wadhamini MOI kitaendelea kesho Septemba 04, 2025.