Watumishi MOI wapewa mkono wa krismasi na mwaka mpya 2026

Na Amani Nsello- MOI

Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetoa zawadi za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2026 kwa watumishi wake, ikiwa ni sehemu ya kuwashukuru kwa utoaji wa huduma bora kwa mwaka 2025 na kuwapa motisha ya kufanya vizuri zaidi katika mwaka 2026.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa zawadi hizo, leo Jumanne Desemba 23, 2025 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Lemeri Mchome amesema kuwa uongozi wa taasisi unatambua mchango mkubwa wa watumishi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa, hivyo kuona umuhimu wa kuwashika mkono hasa katika kipindi cha sikukuu.

“Watumishi wetu ni nguzo muhimu ya mafanikio ya MOI… Tumewaandalia zawadi hizi kama ishara ya shukrani na kutambua juhudi zao katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora wakati wote,” amesema Dkt. Lemeri

Ameongeza kuwa uongozi utaendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi ili kuongeza ufanisi na morali kazini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bi, Marry Kayora amesema jumla ya watumishi 1200 wamepatiwa zawadi hiyo ya Krismasi na Mwaka Mpya.

“Zawadi tunazotoa hapa ni mchele kilo tano, mafuta ya kupikia Lita tano na sukari kwa watumishi karibu 1200…zawadi hizi ni utekelezaji wa azimio la Baraza la Wafanyakazi la MOI lililotaka kutoa motisha kwa watumishi wakati wa sikukuu” amesema Bi. Kayora

Mmoja wa watumishi aliyepokea zawadi hizo kwa niaba ya watumishi wote wa MOI, Mfamasia Francis Nsee, amesema zawadi hizo zimeleta faraja na motisha kubwa kwa watumishi, hasa katika kipindi ambacho familia zinasherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

“Zawadi hizi zimetufanya tujisikie kuthaminiwa. Zinatuongezea moyo wa kufanya kazi kwa bidii zaidi na kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa kwa upendo na weledi,” amesema Bw. Francis

About the Author

You may also like these