Huduma za uuguzi kwa wagonjwa wa dharura na mahututi kuboreshwa nchini

Na Erick Dilli- MOI

Wagonjwa wanaohitaji huduma za uuguzi za dharura na mahututi nchini wanatarajia kufaidika na huduma bora za uuguzi baada ya watumishi wa kada hiyo kupatiwa mafunzo maalum yanayolenga kuwapatia huduma stahiki na kwa haraka ili kunusuru maisha yao.

Akifunga mafunzo hayo leo Desemba 19, 2025 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dkt. Lemeri Mchome, amesema kuwa mafunzo hayo yalete mabadiliko katika utoaji huduma kwa wagonjwa wadharura na mahututi wanaofika katika vituo vyetu vya kazi

“Msipofanyia kazi elimu hii mliyopata katika mafunzo haya, itakuwa ni kazi bure. Hivyo nawasihi mtakaporejea katika vituo vyenu, ujuzi huu uwe sehemu ya utendaji kazi wenu wa kila siku ili kuleta mabadiliko,” amesema Dkt. Lemeri

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wauguzi waliopata mafunzo hayo kuwashirikisha wenzao ili kuhakikisha maarifa hayo yanasambaa na kuchangia kuleta mabadiliko ya huduma za afya kwa kwa wagonjwa wadharura na mahututi.

“Elimu mliyopata si yenu pekee. Ni vyema mkaihamisha kwa watoa huduma wenzenu ili kuleta mabadiliko chanya na ya kudumu katika utoaji wa huduma,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango wa Taasisi ya Elimu ya Huduma za Dharura (EMSA) ameishukuru Taasisi ya MOI kwa ushirikiano endelevu, akisema mafunzo hayo anaamini yanazidi kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha ufanisi kwa wauguzi katika sekta ya afya, hususani katika huduma za dharura.

Naye, mmoja wa wauguzi walioshiriki mafunzo hayo, Bi. Mwanawaziri Ahmad kutoka Hospitali ya Tindwa, amesema mafunzo hayo yameongeza ujuzi na uelewa wake katika kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi.

“Mafunzo haya yameniongezea maarifa na ujasiri zaidi. Naahidi kuyatumia kikamilifu katika majukumu yangu ya kila sikuh ili kuhakikisha wagonjwa wa dharura na maututi wanazidi kupata huduma bora,” amesema Bi. Ahmad.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliwakutanisha wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini, zikiwemo Taasisi ya Jakaya Kikwete ya Moyo (MOI), Hospitali ya Rufaa ya Bugando pamoja na Hospitali ya Tindwa, yakilenga kuboresha ubora wa huduma za uuguzi katika mazingira ya dharura na wagonjwa mahututi.

About the Author

You may also like these