Na Abdallah Nassoro-MOI
Wataalam wa kada ya uuguzi nchini wameshauriwa kuanza kufanya tafiti za namna bora ya kuwahudumia wagonjwa zitakazikidhi vigezo vya mazingira na hali halisi ya Kitanzania badala ya kuendelea kutumia tafiti za maeneo mengine Duniani.
Ushauri huo umetolewa leo Desemba, 15, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe: Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua mafunzo ya huduma bora za uuguzi kwa wagonjwa wa dharura na mahututi yanayoendela MOI.
Amesema ni vyema kwa wataalam wa kada hiyo ya uuguzi kuanza kufanya tafiti zitazozingatia hali halisi ya mazingira ya Kitanzania ili kuboresha utoaji wa huduma dharura na wagonjwa mahututi nchini.
“Mnatakiwa kuanza kufanya tafiti, mchapishe hatupaswi kuwa watumiaji wa tafiti za maeneo mengine, tuanze kufanya tafiti zitakazozingatia mazingira yetu, wagonjwa wa kuwafanyia hizo tafiti wapo ni suala la uamuzi tu” amesema Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa
“Mazingira ya uingereza sio sawa na hapa, mazingira yanatofautiana, kwahiyo ikiwa tafiti iliyochapishwa ni ya sehemu fulani haina maana huwezi kufanya tafiti kama hiyo Dar es Salaam kwasababu mazingira tofauti…hii itasaidia sana kuboresha huduma zetu”
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MOI, Elizabeth Mbaga amesema mafunzo hayo yaliyoshirikisha wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini yana lengo la kuboresha hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi.
Naye Mkurugenzi wa Mipango wa Taasisi ya Elimu ya Huduma za Dharura (EMSA) Ebony Ford amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya MOI na taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo wauguzi katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
“Tangu 2020 hadi leo miaka mitano sasa tumekuwa tukishirikiana na MOI katika kuwajengea uwezo wauguzi kukuza ujuzi wao, sasa tunaangazia huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi, tunajivunia ushirikiano huu kwani unaboresha hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa” amesema Ford