Na Amani Nsello- MOI
Ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamerudhishwa na ubora wa huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo.
Akizungumza Desemba 12, 2025 katika eneo la kusubiria huduma Bi. Asha Juma amesema kwamba ameridhishwa na huduma za MOI, akirejea namna ambavyo wataalamu walivyomhudumia mgonjwa wake aliyepata ajali ya pikipiki na kwa sasa anaendelea.
“Huduma za hapa MOI ni nzuri… Nilimleta mdogo wangu alipata ajali ya pikipiki manesi na madaktari walimhudumia vizuri sana, kwa sasa anaendelea vizuri na leo tumekuja kwa ajili ya kliniki” amesema Bi. Asha
Naye, Bw. John Joseph, ndugu wa mgonjwa aliyelazwa kwa tatizo la mgongo, amesema utaratibu wa mapokezi na maelekezo ya kitabibu kutoka kwa wataalamu umempa imani juu ya matibabu anayopata baba yake.
Kwa upande wake, Bi. Bupe Ngunule, Afisa Muuguzi Mwandamizi kutoka Kitengo cha Udhibiti Ubora MOI, amewaasa ndugu wa wagonjwa wote kuzingatia usiri wa wagonjwa kwa kutochukua picha au video katika maeneo ya Wodi bila ruhusa maalum, ili kulinda faragha na haki za wagonjwa.