Na Abdallah Nassoro- MOI
Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeeleza kuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi ya taasisi hiyo inayolenga kupanua maeneo ya utoaji huduma na kupunguza msongamano wa wagonjwa wa nje (OPD), katika eneo la sasa la kutolea huduma.
Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo CPA Augustino Mbogela amebainisha hayo leo Novemba 27, 2025 baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa jengo lililokuwa hospitali ya Tumaini (X-Tumaini) na ujenzi wa kituo cha utengamao kilichopo Bweni jijini Dar es Salaam.
“Miradi hii licha ya kuwa itasogeza huduma karibu na jamii lakini pia itapunguza msongamano wa wagonjwa wa nje katika eneo la sasa la kutolea huduma…niseme tumeridhishwa na kasi ya ujenzi na nitoe rai kwa wakandarasi kuzingatia muda ili wagonjwa waweze kufaidika na huduma hizi” amesema Mbogela na kuongeza kuwa
“Unapopanua huduma unaruhusu kuwafikia watu wengi zaidi, lakini hii inakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma hizo, naipongeza Menejimenti kwa utekelezaji wa miradi hii, ni imani yangu kuwa mara itakapoanza kufanya kazi basi kila mmoja wetu atashuhudia matunda ya uwekezaji huu”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema mradi wa ukarabati wa X-Tumaini utekelezaji wake umefikia asilimia 96 na kwamba mwanzoni wa Januari 2025 utoaji wa huduma unatarajia kuanza.
“Hapa tutatoa huduma za wagonjwa maalum na wakimataifa, kwa sasa huduma hizi zinatolewa katika eneo dogo pale MOI na kusababisha msongamano wa wagonjwa, lakini kukamilika kwa jengo hili kunafungua njia ya huduma za wagonjwa maalum na za kimataifa kufurahia huduma katika jengo hili” amesema Dkt. Mpoki
Ameongeza kuwa “Hapa zitaendeshwa kliniki na pale mgonjwa atakapolazimika kulazwa basi atapelekwa kwenye wodi zetu…pia mradi wa kituo cha utengamao Bweni kama ulivyo huu, ni mradi wa kimkakati wa kujaribu kusogeza huduma karibu na watu wa eneo hilo ambapo huduma za kibingwa na bobezi zitatolewa pamoja na huduma za utengamao”.