Na Abdallah Nassoro-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kuendesha kambi maalum ya uchunguzi kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi bure ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya watoto wenye changamoto hiyo Duniani.
Zoezi hilo litaanza siku ya Ijumaa tarehe 24 Oktoba, 2025 katika eneo la kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) MOI likiwa na lengo la kuwaibua watoto wapya wenye changamoto hiyo na kufanya ufuatiliaji kwa watoto waliowahi kupatiwa matibabu.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba, 23, 2025 na daktari bingwa wa ubongo wa MOI ambaye pia ni Meneja wa Huduma za Watoto Dkt. Hamisi Shabani ambaye amebinisha kuwa uchunguzi huyo utafuatiwa na huduma za matibabu kwa watakaobainika kuhitaji huduma hizo.
“Baada ya uchunguzi watakaobainika kuhitaji matibabu zaidi ikiwamo upasuaji watafanyiwa bure kutokana na uwepo wa ufadhili wa taasisi ya MO Dewji Foundation na wadau wengine, hivyo hakuna sababu ya mzazi wa mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi kusita kuleta mtoto kwa uchunguzi” amesema Dkt. Shabani
Ameongeza kuwa “Kwa Tanzania kila vizazi 1000 watoto Watatu hupata tatizo hilo, kwa mwaka watoto 4,800 hupata tatizo hilo…sababu kubwa ni utapiamlo unaosababishwa na mama mjamzito kukosa madini ya folic kabla ya ujauzito”
Amesema tatizo hilo linazuilika kwa kuhakikisha mama anahudhuria kliniki ya mama na mtoto ili kupata ushauri kabla ya kubeba ujauzito ikiwa pamoja na kula mboga za majani, mayai na jamii ya mizizi.
“Pia mama anaweza kwenda kununua vidonge vya folic kwenye maduka ya dawa pamoja na vyakula vilivyoongezewa virutubisho hivyo…hata hivyo lengo la uchunguzi huu ni kuwezesha utambuzi na matibabu endelevu ya watoto hao” amesisitiza Dkt. Shabani
Ametoa wito kwa wazazi wa watoto wenye chngamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi kuwaleta watoto kwa ajili ya uchunguzi ili kufungua dirisha la matibabu ya awali na matibabu endelevu kwa watoto waliowahi kutibiwa.