Dkt. Mpoki: Waleteni wazee tuwahudumie

Na Amani Nsello- Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, leo Alhamisi Oktoba 16, 2025, amefungua rasmi kambi maalum ya matibabu kwa wazee katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wazee duniani.

Kambi hiyo imeandaliwa na Taasisi ya MOI ikiwa na lengo la kutoa huduma za kibingwa kwa wazee ambao mara nyingi hukosa fursa ya kupata huduma hizo kwa wakati.

Akifungua kambi hiyo , Dkt. Mpoki amesema kuwa huduma hizo zitakuwa bure kwa wazee wasio na bima na kwa wenye bima, bima zao zitatumika, huduma zitahusisha uchunguzi na matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishapa ya fahamu pamoja na ushauri wa tiba lishe bora kwa wazee na mazoezi tiba.

“Huduma hizi ni maalum kwa ajili ya kuwahudumia wazee wetu waliolitumikia taifa kwa uaminifu. Ni wajibu wetu kama sekta ya afya kuhakikisha tunawajali na kuwapatia huduma stahiki kwa heshima wanayostahili,” amesema Dkt. Mpoki.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali kupitia taasisi zake za afya inaendelea kuboresha huduma kwa makundi maalum kama wazee, na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi

Naye, Daktari kutoka idara ya upasuaji wa ubongo MOI, Dkt. Manase Ng’wenzi amesema kuwa moja ya changamoto wanazokutana nazo kwa wazee ni kuchelewa kufika hospitalini, hali inayosababisha matatizo mengi kuwa makubwa zaidi kuliko yanavyopaswa kuwa.

“Wazee wengi huja hospitali wakiwa tayari wana hali mbaya, lakini kupitia kambi hii, tunalenga kuwafikia mapema na kutoa matibabu ya haraka kabla magonjwa hayajawa sugu,” amesema Dkt. Manase

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi waliofika kupata huduma katika kambi hiyo, Mzee Hamisi Ally (65), mkazi wa Ilala, ameipongeza serikali na MOI kwa kuandaa kambi hiyo huku akieleza kuwa mara ya mwisho kupata vipimo vya afya ilikuwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

“Hii huduma ni msaada mkubwa kwetu. Mimi nilikuwa nashindwa kwenda hospitali mara kwa mara kwa sababu ya fedha. Leo nimefanyiwa mazoezi tiba, nimepimwa na kisukari na nimepewa ushauri mzuri wa lishe,” amesema Mzee Hamisi

Taasisi ya MOI imekua ikiratibu matukio mbalimbali ya kusogeza huduma zake za kibingwa na kibobezi karibu na wananchi.

About the Author

You may also like these