Na Mwandishi Wetu Maalum- COMORO (Anjouan)
Daktari bingwa wa Mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Dkt. Tumaini Minja kwa kushirikiana na wahudumu wa chumba cha upasuaji katika hospitali ya Hombo, kisiwa cha Anjouan nchini Comoro, amefanikiwa kuwafanyia upasuaji watoto wawili waliokuwa na changamoto za mifupa.
Upasuaji huo umefanyika Oktoba, 9, 2025 ambapo ni sehemu ya kuwajengea uwezo wataalam wa afya katika hospitali hiyo namna ya kutoa matibabu kwa njia ya upasuja.
Akizungumza baada ya upasuaji huyp Dkt. Minja amesema ni faraja kwake kuwa sehemu ya timu iliyoshiriki kuwajenga uwezo wa kufanya upasuaji wataalam wa hospitali ya Hombo na kwamba ni imani yake ujuzi huo utaendelea kusaidia wananchi wa kisiwa hicho.
“Kikubwa hapa ni kuwajengea uwezo wataalam wa hapa ili waweze kutoa matibabu ya upasuaji kwa ufanisi…leo tulikuwa na kesi mbili, mmoja mtoto wa miaka Saba (7) aliyevunjika mkono ambapo tumemuwekea chuma na mwingine mtoto wa miaka Minane (8) aliyekuwa na uvimbe mkononi, uvimbe huu ameishi nao kwa miaka miwili” amesema Dkt. Minja
Daktari wa mifupa katika Hospitali ya Hombo Dkt. Hamidi amesema kushiriki katika upasuaji huo kumemuongezea ujuzi na mbinu mpya za kuwatibu wagonjwa wenye mivunjiko.
“Hili ni jambo la kufurahisha kwangu maana nimejifunza mbinu mpya za upasuaji na matibabu ya mifupa, kambi kama hizi ni muhimu kwetu katika kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo, kwa kweli leo ni mtu mwenye furaaha” amesema Dkt. Hamidi
Katika kambi hiyo maalum ya matibabu MOI imeambatana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Kansa ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Makao Makuu ya nchi Dodoma.