Wafanyakazi wa AU kuanza kupata matibabu MOI

Na Amani Nsello- MOI

Wajumbe kutoka Umoja wa Afrika (AU) wametembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), kwa ziara maalum ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, ikiwa ni hatua ya awali kabla ya kuanza kwa mpango wa watumishi wa AU kuanza kupata matibabu katika Taasisi ya MOI.

Wajumbe hao walitembelea Taasisi ya MOI jana Jumatano Oktoba 08, 2025 na kutembelea vitengo vya radiolojia, Kliniki ya wagonjwa wa kimataifa na wodi za ‘Private’

Akizungumza baada ya kukagua miundombinu na huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo, Dkt. Adam Issa, Mkurugenzi wa Tiba na Mambo ya Afya AU alisema wamevutiwa na ubora wa huduma za kisasa zinazotolewa na wataalamu wa MOI.

“Tumejionea wenyewe jinsi Tanzania ilivyopiga hatua katika huduma za afya. MOI ina vifaa vya kisasa, wataalamu wabobezi, na mazingira mazuri kwa wagonjwa. Hivyo, tunakwenda kukamilisha mchakato wa mkataba wa ushirukiano ili wagonjwa kutoka nchi wanachama waanze kuja hapa kupata huduma,” alisema Dkt. Adam

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Anthony Assey alisema ujio wa wajumbe hao ni heshima kubwa kwa taasisi na Tanzania kwa ujumla.

“Ziara hii inaonyesha namna ambavyo juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta matokeo makubwa katika kuboresha huduma za afya…Tuko tayari kupokea wagonjwa Au na mataifa mbalimbali ya Afrika,” alisema Dkt. Anthony

Nae Mkuu wa Divisheni Huduma za Tiba AU Dkt. John Rwegasha alisema mpango huo ni sehemu ya jitihada za Umoja wa Afrika kuimarisha ushirikiano wa katika sekta ya afya ndani ya bara, kwa kutumia vituo vya tiba vilivyo na ubora wa kimataifa.

“Tunataka wananchi wa Afrika wapate huduma bora bila kulazimika kwenda nje ya bara letu. MOI ni mfano mzuri wa mafanikio hayo,” alisema Dkt. Rwegasha

MOI imekuwa ikitambulika kama moja ya vituo bora vya tiba barani Afrika, ikitoa huduma za kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo, ajali, mishipa ya fahamu na magonjwa ya ajali kwa wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali.

About the Author

You may also like these