MOI yatoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa 117 siku ya kwanza kambi ya matibabu comoro

Na Mwandishi Wetu- Anjouan-COMORO

Madaktari bingwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamefanikiwa kutoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa 117 siku ya kwanza ya kambi maalum ya matibabu katika kisiwa cha Anjouan nchini Comoro, huku wagonjwa hao wakiishukuru Tanzania kwa kusogeza huduma karibu yao.

Daktari bingwa wa Mifupa wa MOI, Dkt. Tumaini Minja amesema hayo leo Oktoba, 05, 2025 kuwa kati ya wagonjwa hao, 89 wa mifupa na wagonjwa wengine 28 wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.

“Huduma tunazitoa katika hospitali mbili, wapo madaktari wanaotoa huduma hapa hospitali ya Hombo na wengine Bambao…kwa ujumla wake tumekuwa na siku nzuri ya kuanza kutoa matibabu kwa wananchi wa kisiwa hiki cha Comoro” amesema Dkt. Minja

Amefafanua kuwa “Kutoka na takwimu za leo ni wazi kuwa watu wengi hapa Anjouan wanachangamoto za mifupa zinazotokana na ajali na uzee, wanahitaji matibabu ya kibingwa kutatua changamoto hizo, wapo wanaohitaji matibabu ya upasuaji, hao tumewapa rufaa ili waje MOI kwa matibabu zaidi na wengine wasiohitaji tiba ya upasuaji tumewapa dawa”

Abdallah Yousuf ambaye ni miongoni mwa wagonjwa waliopatiwa matibabu na madaktari bingwa wa MOI katika kambi hiyo ameishukuru Tanzania kwa kuleta madaktari hao ili kuwasogezea karibu huduma za kibingwa.

“Naishukuru Tanzania kwa huduma hii, sio wote wenye uwezo wa kusafiri hadi Tanzania kufuata huduma za kibingwa, leo nimetibiwa nikiwa hapa nyumbani na bila gharama zozote, kwa hakika ni jambo la kufurahisha sana” amsema Yousuf

Katika kambi hiyo maalum ya matibabu MOI imeambatana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa (MNH), Taaisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Kansa ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Makao Makuu ya nchi Dodoma

About the Author

You may also like these