Na Amani Nsello- MOI
Ikiwa Wiki ya Ustawi wa Jamii Kitaifa ikiendelea kuadhimishwa kuanzia tarehe 25 hadi 30 Agosti 2025 katika viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam chini ya kauli mbiu “Pata Msaada wa Kisaikolojia; Imarisha Afya ya Akili,” Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetambua umuhimu wake kwa kutoa mafunzo maalum kwa watumishi wake.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uelewa juu ya nafasi na majukumu ya Afisa Ustawi wa Jamii hospitalini, ili kila mtumishi aweze kushirikiana ipasavyo katika kuwahudumia wagonjwa wenye changamoto za kijamii na kisaikolojia.
Mafunzo hayo yalifunguliwa Agosti 27, 2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MOI, Bw. Fidelis Minja ambaye alisema kwamba ni vema kwa kila mtumishi kufahamu majukumu ya Afisa Ustawi wa Jamii ili kuweza kutoa huduma bora kwa wagonjwa wenye mahitaji ya kijamii.
“Ni muhimu kila mtumishi kumfahamu Afisa Ustawi wa Jamii anafanya nini?… ili tuwajue mapema wagonjwa wenye changamoto kubwa kabla gharama za matibabu hazijawa kikwazo,” alisema Bw. Minja
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa MOI, Bi. Stella Kihombo alieleza kwa kina majukumu makuu ya kada hiyo, ikiwemo kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, kufanya tathmini ya kijamii na kiuchumi, kufuatilia wagonjwa majumbani (outreach), kuunganisha wagonjwa na familia zao pamoja na kusimamia sera ya msamaha wa matibabu.
“Wapo wagonjwa wanaopoteza viungo kutokana na upasuaji, hawa wanahitaji msaada mkubwa wa kisaikolojia ili kuimarisha afya ya akili na kuendelea na maisha yao,” alisema Bi. Stella
Naye, Bi. Furaha Godfrey, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, alisema kupitia mafunzo hayo yamemjengea uwezo wa kutambua mchango mkubwa wa Afisa Ustawi wa Jamii katika masuala ya afya na tiba kwa ujumla.