Banda la MOI laendelea kuwa kivutio maonesho ya nanenane dodoma

Na Amani Nsello- DODOMA

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa wa Dodoma na jirani wameendelea kujitokeza kwa wingi katika banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika maonesho ya wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.

Katika banda hilo, wananchi wanapata huduma za ushauri wa kitaalamu kuhusu matatizo ya mifupa, ubongo, mishipa ya fahamu, uti wa mgongo, tiba lishe , Fiziotherapia na elimu ya kujikinga dhidi ya maradhi hayo.

Akizungumza katika maonesho hayo, leo Jumapili Agosti 03, 2025 Daktari wa mifupa wa MOI, Dkt. Angela Mlingi amesema kuwa mwitikio ni mkubwa kwa wananchi ambao wanaendelea kujitokeza kwa wingi katika banda hilo na wanawapa ushauri kuhusu afya zao.

“Tunaendelea kutoa huduma za ushauri na uchunguzi wa awali kwa wananchi… Mwitikio ni mkubwa sana na wananchi wanaonyesha kiu kubwa ya kutaka kupata maarifa kuhusu matatizo ya mifupa na ubongo” amesema Dkt. Angela na kuongezea

” Wananchi wajitokeze kwa wingi kwa kuwa elimu ya afya ni msingi wa kinga katika maisha ya binadamu”

Naye, mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Bw. John Kusuza kutoka Chamwino amesema kuwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo kwa muda mrefu, lakini leo amepata ushauri mzuri kutoka kwa madaktari wa MOI.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025” yalianza Agosti 01 na yatafikia tamati Agosti 08, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.

About the Author

You may also like these