Katibu mkuu wizara ya afya aipongeza MOI kwa kutoa huduma bora za kibingwa na kibobezi kwa watanzania

Na Abdallah Nassoro- MOI

Katibu Mkuu Wizara ya Afya ameipongeza Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kuendelea kutoa huduma bora za kibingwa na kibobezi za matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania.

Pongezi hizo zimetolewa Julai, 30, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Seif Shekalaghe alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua hali ya utoaji huduma MOI.

Amesema “Wizara inaipongeza MOI kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya , tunatambua kazi yenu na tunathamini…endelezeni umoja, mshikamano na upendo sehemu ya kazi ili mzidishe jitihada katika kuwahudumia Watanzania hawa”

“Tumeongea na wananchi pale, nao wanawapongeza, hili ni jambo la kujivunia, hakikisheni hizi kero ndogondogo mnaziondoa kwa haraka…Suala la kupanua ICU ni jambo muhimu sana, kwasababu kuna watu wanalazimika kusubiri kufanyiwa upasuaji kwa wiki mbili akisubiri kitanda cha ICU, sisi wizara tupo tayari kuwaunga mkono, pamoja na lile la ICU ya watoto”

Aidha Dkt. Shekalaghe amesema ni muhimu kwa taasisi hiyo kuendelea kuwajengea uwezo madaktari wa hospitali za mikoa na kanda ili wagonjwa katika maeneo hayo wasilazimike kufika MOI kwa matibabu na badala yake waende katika hospitali hizo.

“Nimeambiwa kwa siku munapokea wagonjwa 500 kati ya hao 150 pekee ndiyo wanasifa za kuja kutibiwa MOI na 350 wangeweza kutibiwa katika hospitali za mikoa na kanda, sasa niwaombe muwajengee uwezo hospitali za Dar es Salaam kwanza, hii itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa hapa MOI” amesisistiza Dkt. Shekalaghe

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya Dkt. Ahmad Nyembea amesema serikali imewekeza miundombinu na vifaa tiba katika hospitali za za mikoa, kanda na taifa ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora karibu na maeneo yao na kwamba ni jukukumu la MOI kuwajengea uwezo wataalam katika hospitali hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisya ameeleza kuwa MOI inaishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma MOI pamoja na kuwalipa mishahara watumishi pamoja na kuwajengea uwezo wataalam kupitia mafunzo SET ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Mpoki amemueleza katibu mkuu kwamba, Taasisi ya MOI imeyapokea malekezo yote na kwamba menejimenti itakwenda kuyafanyia kazi na taarifa zitawasilishwa wizarani kama ilivyoelekezwa.

Akiwa katika taasisi ya MOI Dkt. Shekalaghe ametembelea wodi namba 5B ya watoto wenye vichwa vikubwana mgongo wazi, ICU, OPD, Chumba cha Upasuaji, mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wan je na vyumba vya upasuaji na kuongea na sehemu ya watumishi wa MOI.

About the Author

You may also like these