Na Erick Dilli- SABASABA
Wananchi 1,908 wametembelea Banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara, Sabasaba 2025 yaliyomalizika leo Julai, 13,2025
Hayo yamebainishwa Julai 13, 2025 katika kilele cha Maonesho hayo na Daktari bingwa Mbobezi wa Mifupa MOI, Dkt. Tumaini Minja ambapo amesema wanamchi wenye changamoto za Mifupa, Ubongo, mgongo, nyonga, magoti wamenufaika na huduma hizo zilizotolewakwa gharama nafuu pamoja na kupata elimu.
“Jumla ya wananchi 1,908, wametembelea katika Banda letu, kati ya hao 455 wamepatiwa matibabu na 1,503 wamepatiwa elimu ya afya wakati wa maonesho haya…tulikuwa na sehemu mbili, ya matibabu yaani kliniki na maonesho ambapo wananchi walipata ushauri kutoka kwa watalaam wa lishe, viungo saidizi na Muuguzi kutoka chumba cha upasuaji” amesema Dkt. Minja na kuongezea
“Kwa wagonjwa ambao walihitajika kupata vipimo vikubwa vya MRI na CT Scan tumeweza kuwapa rufaa ya kwenda kupatiwa vipimo hivyo katika Taasisi yetu (MOI) kwa lengo la kuhakikisha mgonjwa tunaemuona hapa (Sabasaba) anapatiwa matibabu bora na sawa akifika katika Taasisi yetu”
Aidha, Afisa Muuguzi Mwandamizi MOI Bi. Scholastica Mansillo ameendelea kuhimiza wananchi wenye changamoto ya Mifupa, Mgongo, Ubongo na Mishipa ya fahamu kufika katika Taasisi ya MOI na kupata Matibabu kutoka kwa Madkatari bingwa na bobezi pamoja na Watalaam wengine kutoka Taasisi hiyo.