Watumishi MOI washerehekea siku yao maalum – ‘MOI DAY 2025’

Na Amani Nsello- KUNDUCHI

Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wameadhimisha kwa furaha na sherehe maalum siku ya ‘MOI DAY 2025’ , tukio linaloadhimisha mafanikio makubwa ya taasisi hiyo katika kutoa huduma bora za Kibingwa na Kibobezi za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu kwa wananchi takribani miaka 29 tangu kuanzishwa kwake.

Sherehe hiyo imefanyika leo Julai 06, 2025 katika Hoteli ya SilverSands, Bahari Beach, Kunduchi Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Anthony Assey ambaye amesema kwamba ‘MOI DAY’ ni siku muhimu ya kutafakari mafanikio, changamoto na dira ya taasisi hiyo katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Leo tunasherehekea mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu… Hii pia ni siku ya kuwashukuru watumishi wa MOI kwa kujitoa kwao kila siku kuokoa maisha ya wananchi” amesema Dkt. Anhony

Dkt. Antony pia ameishukuru kamati ya maandalizi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Orest Mushi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kwa kufanikisha siku hiyo maalum kwa watumishi wa taasisi hiyo.

Miongoni mwa matukio ya kuvutia yalikuwa ni michezo ya watumishi ikiwemo mpira wa miguu ambapo Mashabiki wa Yanga wanaume waliibuka na ushindi kwa kuwatandika Simba mabao ma3 kwa 0, Mashabiki wa Yanga wanawake waliwafunga Simba penati 3 kwa 0.

Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba Mashabiki wa Yanga wanawake waliibuka na ushindi huku Mashabiki wa Simba wanaume wakiibuka na ushindi.

About the Author

You may also like these