Banda la MOI laendelea kuwa kivutio katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma dodoma

Na Erick Dilli – Dodoma

Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameendelea kutembelea banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na kupata elimu kuhusu huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa na Taasisi hiyo.

Akiongea na viongozi hao leo Juni 23, 2025 Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu MOI Bw. Orest Mushi, akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MOI katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma, Viwanja vya Chinangali Park, Jijini Dodoma, amewaeleza huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo ikiwemo na huduma mpya zilizoanzishwa.

“Taasisi ya MOI inatoa huduma za kibingwa na kibobezi kwenye maswala ya Mifupa, Mgongo, ubongo na Mishipa ya fahamu ambapo tunamadaktari bingwa na watalaam wakutosha waliobobea katika fani hiyo” amesema bw. Orest na kuongezea

“Taasisi yetu imefanikiwa kuanzisha huduma mpya kumi (10) za kibobezi ikiwemo upasuaji wa mgongo kupitia tundu dogo, upasuaji na uchunguzi wa ubongo bila kufungua fuvu, upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde, matibabu ya maumivu sugu ya mgongo, upasuaji wa ubongo kwa kutumia mawimbi ya sauti na upasuaji wa kutibu kiharusi.’’

Naye, Daktari kutoka Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya fahamu MOI Dkt. Manase Ng’wenzi amewaeleza viongozi kuhusu huduma yetu ya kliniki ya wagonjwa maalam na wakimataifa ambapo maelfu ya wagonjwa kutoka nje ya Tanzania wamehudumiwa.

Akitoa ushuhuda kuhusu huduma bora za MOI Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Taasisi, kutoka Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda amewashukuru na kuwapongeza Watumishi wa MOI kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi.

About the Author

You may also like these