Na Stanley Mwalongo- DODOMA
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameipongeza Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa juhudi na kazi nzuri ya kutoa huduma bora za kibingwa na kibobezi kwa wananchi.
Mhe. Katambi amesema hayo leo Juni 3, 2025 alipotembelea banda la MOI katika viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma ambapo amesema juhudi zinazofanywa na watumishi wa MOI katika kutoa huduma ni zaidi ya utaalam ila ni wito.
“Licha ya kazi yenu kuwa ya kitaalam ila ni wito na ni zaidi ya kujitoa hivyo hongereni sana na nimeona nije niwasalimie kwani sio lazima tuwe wagonjwa ndio tuje kuwaona hapana hata tukiwa wazima tunafurahi pamoja na nyie” amesema Mhe. Katambi.
Pia, Mhe. Katambi amepongeza kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Taasisi ya MOI ili kuzidi kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Aidha, Mhe. Katambi amesema anatambua Taasisi ya MOI imekuwa ikiwahudumia vizuri walemavu mbalimbali kwa kuwatengenezea viungo saidizi ambavyo vinavyowasaidia kurejea katika hali zao za kawaida.