Emma kiduku charity group wachangia matibabu ya watoto 6 wenye kichwa kikubwa MOI

Na Amani Nsello- MOI

Kikundi cha Hisani cha Emma Kiduku Charity Group kimechangia matibabu ya watoto 6 wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi wanaotibiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Ubongo Muhimbili (MOI).

Kikundi hicho kilikabidhi msaada huo Mei 4, 2025 MOI, ambapo kiongozi wa kikundi hicho Bw. Emmanuel Madaha amesema lengo la kutoa msaada huo ni kusaidia kufanikisha matibabu ya watoto hao ambao wengi wao wanatokea kwenye familia duni na zisizojiweza kiuchumi.

“Tumekuja hapa kwa lengo la kusaidia watoto hawa wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa sababu wengi wao wanatoka familia zenye uchumi duni hivyo kushindwa kumudu gharama za matibabu yao” alisema Bw. Emmanuel

Aidha, Bw. Emmanuel aliongeza kwa kusema kuwa licha ya kuchangia matibabu ya watoto hao lakini pia walitoa sabuni za maji lita 40 kwa ajili ya matumizi ya watoto hao.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Msaidizi wa MOI, Bw. Yosephu Kuruba amesema MOI hupokea watoto wengi kutoka sehemu mbalimbali wakiwa hawana uwezo wa kuchangia gharama za matibabu, kupitia msaada huo utawasaidia watoto hao kufanikisha matibabu yao.

“Tunapokea watoto kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wengi wao wakiwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu. Hivyo msaada huu sio tu umeokoa maisha, bali umeleta matumaini mapya kwa familia nyingi,” alisema Bw. Yosephu

About the Author

You may also like these