Mashabiki wa simba sc wachangia damu MOI

Na Erick Dilli- MOI

Mashabiki wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Simba wamejitokeza kwa wingi kuchangia damu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili MOI.

Zoezi hilo limefanyika leo Aprili 19, 2025 ambapo Mashabiki wa Simba wamejitokeza kuchangia damu MOI kwa lengo la kuokoa maisha ya watanzani pamoja na kuunga mkono timu yao kesho dhidi ya Stellenbosch FC.

Mmoja wa Washabiki wa Timu hiyo Bw. Amiri Yussuf ameeleza lengo la kuchangia damu pamoja na kuhamasisha wadau wa timu hiyo kuelekea mechi yao ya kesho.

“Swala la kuchangia damu lina faida nyingi lakini moja wapo ni kuokoa maisha ya watanzania, kwani tunafahamu kuna ongezeko la wagonjwa MOI wanaohitaji damu na tumeona ni vyema kufanya hilo” amesema Bw. Amiri na kuongezea

“Kuelekea mechi dhidi ya wapinzani wetu siku ya kesho nitoa rai kwa wadau kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuiunga mkono timu yetu ili ivuke hatua hii na kuelekea fainali”

Mratibu wa Timu ya Damu salama MOI Bw. Mohamed Kadeshi amewashukuru mashabiki hao na kutoa rai kwa wengine kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa tiba ya damu.

“Nipende kuwashukuru mashabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Simba kwa moyo na uthubutu wenu kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa Watanzania wenzetu… lakini pia nitoe rai kwa wadau wengine kujitokeza kwani uhitaji wa damu bado ni mkubwa” amesema Bw. Kadeshi

About the Author

You may also like these