Na Stanley Mwalongo- MOI
Kampuni ya SANKU imetembelea kitengo cha Tiba lishe na watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi katika Taasisi ya tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa lengo la kushirikiana katika kukabiliana tatizo hilo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Machi 25, 2025 katika wodi ya watoto 5 MOI, Meneja Mashirikiano wa Kampuni ya SANKU Gwao Omari Gwao amesema wametembelea MOI ili kuangalia namna gani wagonjwa hao wanavyohudumiwa na changamoto zipi wanapitia ili washirikiane na MOI kukabiliana na tatizo hilo.
“Ujio wetu hapa ni kutembelea kitengo cha tiba lishe na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanaotibiwa MOI ili kuanzisha ushirikiano ambao utajikita zaidi kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya vyakula venye virutubisho na unga wenye madini ya folic, Zin na B9 kwa lengo la kuzuia hili tatizo la kichwa kikubwa” amesema Gwao
Gwao amesema watashikiana na wataalam wa MOI kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo mbalimbali kwa kwenda mikoani ili wawafikie watanzania wengi zaidi.
Kwa upande wake Afisa Tiba lishe, Germana Gasper amesema kupitia ushirikiano huo MOI itazidi kuboresha huduma zake kwa wagonjwa wake wake wenye matatizo ya vichwa vikubwa, pia wazazi watapewa elimu ya kutumia vyakula ambayo vipo karibu yao ili kuzuia tatizo hilo.