MOI yatoa huduma za kibingwa kwa washitiri na wakazi wa mbeya

Na Abdallah Nassoro-Mbeya

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepiga kambi ya kutoa huduma za kibingwa za ushauri wa mifupa , ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu na magonjwa ya ndani katika mkutano wa 109 wa Washitiri wa vipindi vya elimu kwa umma unaofanyika ukumbi wa City Park jijini Mbeya ambapo wakazi wa jiji hilo wamejitokeza kwa wingi kupata matibabu hayo.

Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Meneja Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi amesema MOI inatoa huduma hizo kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) ambapo huduma hizo zitaendelea kutolewa hadi Ijumaa Februari 21, 2025.

“Ni fursa kwa washitiri kuchunguza afya zao, lakini pia ni fursa kwa wakazi wa Mbeya kuja kupata huduma za kibingwa na kibobezi za matibabu ya mifupa, ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu na magonjwa ya ndani…tumeamua kusogeza huduma hizi karibu na washiriki wa mkutano na wananchi ili kupanua wigo kwao wa kupata huduma za kibingwa” amesema Mvungi na kuongeza kuwa

“Huduma hizi zimeanza Siku ya Jumatatu Februari 17, na zitatolewa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni…wananchi wote wanakaribishwa kuja kuchunguza afya zao wale wataohitaji vipimo na dawa wataenda kupata vipimo hivyo hospitali ya rufaa ya Kanda Mbeya MZRH”

Baadhi ya wanufaika na huduma hizo wameipongeza MOI kwa kusogeza huduma za kibingwa karibu na washitiri wa mkutano huo na wananchi, kwa kuwa wengi wao hukosa muda wa kuchunguza afya zao kutoka na kubanwa na majukumu.

“Wengi tunanenda kuchunguza afya hali ikiwa tete, unajikuta umezongwa na majukumu na hata hukumbuki kupima afya hadi utakapoanza kuhisi maumivu mwilini…sasa kwa kitendo hiki nawapongeza sana, kinatukumbusha kuwa pamoja na majukumu yetu basi tujali pia afya zetu” amesema mmoja wa washitiri ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe

About the Author

You may also like these