MOI yazindua matumizi ya teknolojia ya mawimbi ya sauti katika upasuaji wa ubongo

Na Amani Nsello- MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imezindua matumizi ya mawimbi ya sauti wakati wa upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo (High-intensity Focused Ultrasound -HIFU) na kufanya wataalam kutoka nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kuja MOI kujifunza kutumia teknolojia hiyo.

Hayo yamebainishwa Siku ya Jumatatu Februari 17, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua mafunzo ya awamu ya 4 ya Magonjwa ya Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu katika ukumbi wa Mikutano wa Ummy Mwalimu uliopo Hospitali ya Taifa Muhimbili- Upanga.

Dkt. Mpoki amesema teknolojia hiyo inasaidia kufungua sehemu ndogo ya fuvu la kichwa na kumuacha mgonjwa na kovu dogo.

“Huu utaalam wa kutumia mawimbi ya sauti kufuatilia maendeleo ya upasuaji kwa wagonjwa ambao wana uvimbe ndani ya ubongo (intraoperative Ultrasound neuronavigation), uwe wa saratani au wa namna nyingine unaongeza ufanisi katika kuumaliza uvimbe wote. Teknologia hii ni ya kipekee hivyo wengine watakuja kujifunza na wataalam wetu watatumika kama walimu kwa wanafunzi wanaotoka nchi za Afrika Mashariki na Kati na wengine wataopata nafasi ya kutembelea nchi yetu (Tanzania) kwa ajili ya afua hizi”- amesema Dkt. Mpoki na kuongezea

“Maana yake tunaweza kusema mtu yeyote anayekuja hapa Tanzania mwenye changamoto kama hiyo ujuzi huo (Teknolojia ya kutumia mawimbi ya sauti wakati wa upasuaji wa ubongo) utakaotumika kumtibu, miaka yote sisi (MOI) tutakuwa mbele”

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI, Dkt. Laurent Lemeri Mchome amesema MOI imekuwa ikishirikiana na chuo kikuu cha Corolado cha nchini Marekani ambapo wataalamu wa MOI wamekuwa wakienda chuoni hapo kuongeza ujuzi na wataalam kutoka chuo hicho wamekuwa pia wakitenbelea MOI kuwajengea uwezo.

Kwa upande wake, Daktari bingwa mbobezi wa Ubongo, kutoka Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani, Prof. Rayn Ormond ameishukuru Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania ya awamu ya 6 inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa idhini na kibali cha kuendesha mafunzo hayo nchini Tanzania.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, madaktari bingwa wa chumba cha wagonjwa mahututi na waguuzi wabobezi wa chumba cha wagonjwa mahututi.

Mafunzo hayo yameanza leo Jumatatu Februari 17 na yatafikia tamati Februari 21, 2025 na yameandaliwa na kuratibiwa na MOI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani ambapo wataalam kutoka MOI, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Bugando, Hospitali ya Rufaa Kanda- Mbeya, Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila, Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH)- Dodoma na Lugalo wamehudhuria.

About the Author

You may also like these