Na Amani Nsello- MOI
Ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamekumbushwa kufuata utaratibu wa idadi ya watu wa kuwaona na kuwajulia hali wagonjwa wao wanaopatiwa huduma za matibabu.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa Februari 14, 2025 na Mwakilishi wa Meneja Udhibi Ubora wa MOI, Zaituni Bembe wakati akijibu hoja na maoni mbalimbali eneo la kusuniria huduma (MOI Clients Lounge).
Bi. Zaituni amesema kuwa ni muhimu kwa ndugu hao kufuata utaratibu uliopo ili kujikinga na magonjwa lakini pia kuwapa nafasi wauguzi kufanya kazi yao kwa ufasaha.
“Katika taasisi yetu (MOI) tuna utaratibu maalaum wa kuona wagonjwa, tunaruhusu idadi ndogo ya ndugu wa wagonjwa kwa ajili ya kukinga magonjwa ya kuambikiza yatokanayo na msongamano wa watu… Pia kuwapa nafasi zaidi wauguzi wetu kuwahudumia wagonjwa kwa ufasaha”- amesema Bi. Zaituni
Aidha, Bi. Zaituni amewaasa ndugu hao wa wagonjwa kuzingatia uandaaji wa vyakula kwa kufuata matakwa (uhitaji) wa mgonjwa.
Kwa upande wake, ndugu wa mgonjwa Abeid Mwakulasya kutoka Mbeya amewashukuru watumishi wa MOI kwa huduma za matibabu wanazotoa hususani madaktari, wauguzi na wahudumu wa afya.
“Asanteni sana kwa huduna zenu nzuri, tunawashukuru madaktari, manesi na wahudumu wa afya kwakweli mpo vizuri, mpeni salam Dkt. Vaileth Kalinga kutoka kitengo cha Radiolojia mwambieni nashukuru kwa huduma zake” amesema Bw. Abeid