Na Amani Nsello- MOI
Watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), wameshauriwa kujipa muda wa kuwajua wenza wao kabla ya kuchukua uwamzi wa kufunga nao ndoa ili kuepusha migogoro baada ya ndoa inayoweza kuathiri ufanisi kazini.
Ushauri huo umetolewa siku ya Jumatano Novemba, 06, 2024 na Afisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Stella Kihombo wakati akiwasilisha mada ya migogoro ya ndoa inavyoathiri ufanisi kazini wakati wa mafunzo watumishi wa taasisi hiyo.
Bi. Stella amesema kuna hatua nne muhimu za kuzingatia kabla ya wenza kuamua kufunga ndoa ili kupunguza migogoro kwenye maisha ya ndoa.
“Siku hizi kuna tabia imeibuka yaani umekutana na mtu wiki moja wiki ya pili mnafikiria kufunga ndoa, hata hamjajuana, ndoa ina hatua zake, kuna hatua ya mahaba hii huwa kati ya miezi miwili hadi sita, ya pili kufahamiana, ya tatu ni ile ya kukata tamaa, na ya nne ni kujiimarisha” amesema Bi. Stella na kuongezea
“Katika ile hatua ya kwanza ya mahaba ni kipindi ambacho kila unachoambiwa na mwenza (mpenzi) wako unakubali na unaona ni sawa tu, huwezi kuona upungufu wala ubaya wa mwenzako, kuna hatua ya kufahamiana hapo sasa umeshaanza kujua tabia ya mwenzako heeeeh! Kumbe yupo hivi? ni mbahili hivi?…
ni kipindi kigumu sana, kuna kipindi cha kukata tamaa yaani hatua hii ikifika hata hutamani kufunga ndoa maana ushajua tabila halisi za mwenza wako, hatua ya mwisho ni kujiimarisha, hapa ushajua mapungufu yake unayaridhia, pamoja na mabaya yake lakini pia ana mazuri yake hivo mnafanya maamuzi ya kuingia kwenye ndoa”