Na Amani Nsello-MWENGE
Wakazi wa Mwenge Jijini Dar es Salaam wameipongeza Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Kwa kuweka kambi maalum ya matibabu katika Zahanati ya Mwenge na kusogeza huduma hizo karibu yao.
Pongezi hizo zimetolewa Jumanne Oktoba 01, 2024 Siku ya Wazee Duniani na kilele cha kambi hiyo, wakazi wa Mwenge na viunga vyake wameipongeza taasisi ya MOI kwa kusogeza karibu yao huduma. hizo za kibingwa na kibobezi kwa siku tatu mfululizo kuanzia Septemba 29, 2024 hadi Oktoba 01, 2024.
Mmoja wa wagonjwa aliyefika kupata huduma za matibabu Bi. Hadija Omary amesema kuwa anaomba kambi hizo ziwe endelevu kwani zinawapunguzia adha za kufata wataalam katika taasisi hiyo.
“Kambi hii imekuwa msaada kwetu, hususani kwa sisi ambao umri umeenda (wazee), nilisikia tangazo juzi nikasema ngoja nije, tunaomba kambi za namna hii ziwe endelevu kwani zinapunguza usumbufu kwa sisi kuzifuata huko MOI”. Amesema Bi. Hadija
Aidha, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa MOI Dkt. Asha Abdullah amesema kuwa kambi hiyo maalum hiyo katika zahanati ya Mwenge imefanikiwa kwa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 150, hivyo ana matarajio kuwa wataendelea kuwasogezea huduma wagonjwa karibu kwa kuendesha kambi nyingi zaidi.
“Katika siku tatu za kambi yetu hapa Zahanati ya Mwenge tumehudumia zaidi ya wagonjwa 150, tutaendelea kuendesha kambi hizi maalum ili kuwasogezea huduma karibu za kibingwa na kibobeziā¦pia niwaombe wazee muwe na utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuweka viungo vyao imara.” Amesema Dkt. Asha.