Na Erick Dilli-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Mubimbili (MOI) imepokea msaada wa mashine tano za kusaidia wagonjwa kupumua (Ventilators) na viti mwendo viwili kutoka asasi ya kiraia ya African Federation.
Vifaa tiba hivyo vimepokelewa leo Septemba 05, 2024 katika jengo jipya la MOI na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi MOI Dkt. Lemeri Mchome ambaye ameishukuru asasi hiyo ya kiraia kwa kutoa msaada huo kwani vifaa tiba hivyo vitasaidia wagonjwa na kuboresha huduma za matibabu kwa watoto wadogo pamoja na wagonjwa mahututi hospitalini hapo.
“Tunaishukuru asasi hii ya African Federation kwa msaada huu, msaada huu ni muhimu kwetu kwa kuwa utasaidia uzalishaji oxygeni, mashine hizi zitakuwa msaada mkubwa hasa kwenye wodi ya watoto, mapokezi ya dharura, ICU na HDU hivyo itatuongezea ufanisi katika utoaji huduma bora na kuhakikishia wagonjwa usalama wa maisha yao”. amesema Dkt. Lemeri
Awali akikabidhi msaada huo mwakilishi wa asasi ya African Federation, Akhter Khakoo amesema kuwa wao kama asasi ya kiraia wametoa vifaa tiba hivyo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa Taasisi ya MOI na watu wenye ulemavu na mahitaji ya kupumua.
Akiishukuru asasi hii ya African Federation, kaimu mkurugenzi huyo alihamasisha asasi nyingine kutoa misaada ya kijamii kama asasi hii ya African Federation ilivyofanya.