Mhe. Salma kikwete awafariji watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi MOI

Na Stanley Mwalongo- MOI

Mbunge wa Jimbo la Mchinga, mkoani Lindi na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne Mama Salma Kikwete ametembelea, kuwajulia hali, kuwafariji na kuwaunga mkono kwenye shughuli zao za ujasiriamali wakiwa wodini wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanaoendelea na matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbli (MOI).

Mhe. Mama Salma Kikwete leo Agosti, 20, 2024 licha ya kuwafariji kwa kuwapa pole, pia alinunua bidhaa za ususi zinazotengenezwa na wakina mama hao ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono katika jitihada zao za kujikwamua kiuchumi wakati wakiendelea kuwauguza watoto wao.

Kwa upande wao wakina mama wanaouguza watoto wao katika wodi 5B wamemshukuru Mbunge huyo wa jimbo la Mchinga kwa moyo wa upendo na huruma kwa kutenga muda wa kuwajulia hali na kuwaunga mkono katika shughuli zao za ujasiliamali.

“Nashukuru leo mheshimiwa ametutembelea kwaajili ya kutupa pole, tumejisikia vizuri na kufarijika kuona wanatujali pia ameweza kuona kazi ya mikono yangu ya ujasiriliamali ninayofanya hapa nikiwa ninamuuguza mwanangu na amenipa oda ya kumtengenezea mkeka wa meza yake” amesema Bi. Ana Paul

Mzazi Mwingine, Ashura Bakari amemshukuru Mhe. Salma Kikwete kwa kuwaunga mkono na kushuhudia  jinsi gani wakina mama wanajiendeleza na biashara wodini wakiwa wanauguza kwa kutengeneza kacha za mkononi na mikeka ya kuwekea sahani mezani.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amemshukuru Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kwa kuwajulia hali wazazi hao na kusema MOI iko bega kwa bega kuhakikisha watoto hao wanapata matibabu ya kibingwa na kibobezi ili wapone haraka.

About the Author

You may also like these