Na Abdallah Nassoro-MOI
Ujenzi wa jengo jipya la kisasa la ghorofa nne la wagonjwa wa nje (OPD) katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) unatarajia kuanza hivi punde baada ya zoez la kutia saini mkataba wa ujenzi
Taasisi ya MOI jana Agosti 16 2024 imesaini mkataba wa ujenzi na kampuni ya China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co.Ltd kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,000 kwa siku huku ujenzi wake ukitarajia kuchukua miezi 15 na kugharimu Tsh. 10.9 bilioni ambazo asimilia 80 ni kutoka serikalini na asimilia 20 ni mapato ya ndani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini MOI Profesa Charles Mkony amesema mradi wa ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje unakwenda kuweka historia kwa kuondoa changamoto ya msongamano wa wagonjwa wa nje katika Taasisi ya MOI.
“Kazi hii ya ujenzi wa jengo jipya la kliniki ni mradi wa muda mrefu, lengo la ujenzi wa jengo hili ni kupunguza msongamano wa wagonjwa wa nje” amesema Profesa Charles Mkony.
“Hata hivyo serikali yetu ilitangulia kutoa Bilio 1.5 kwa ukarabati wa iliyokuwa Hospitali ya Tumaini ili kutatua tatizo hili kama mpango wa muda mfupi ambapo kazi ya ukarabati imeshaanza na itakamilika ndani ya miezi minne na wagonjwa hawa wataanza kuonwa katika eneo hili wakati mradi wa mda mrefu ukiendelea kutekelezwa” amefafanua mwenyekiti huyo
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi MOI Dkt. Lemeri Mchome amesema kwa sasa sehemu ya kukaa wagonjwa iliyopo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wa nje 250, hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika eneo hilo.
Amesema baada ya ujenzi kukamilika MOI itakua ina uwezo wa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,000 kwa wakati mmoja.
“Leo tumekusanyika hapa kushuhudia utiaji wa saini wa mkataba wa awali wa ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (New OPD), ujenzi wa jengo hilo utakuwa ni wa miezi kumi na tano (15), pia litakuwa la ghorofa nne na vyumba ya kuonea wagonjwa arobaini (40) na kugharimu Tsh. 10.9 bilioni” amesema Dkt. Lemeri
Ameongeza kuwa “Jengo hili linajengwa kwa fedha za Serikali yetu ikiwa asilimia zaidi ya 80 kutoka serekali kuu na asilimia 20 ikitoka katika mapato ya ndani ya taasisi”.
Mwakilishi wa Kampuni ya ujenzi kutoka China Bw. Peng Chao amesema kuwa kampuni yao ina zaidi ya miaka arobaini katika tasnia ya ujenzi hivyo watajenga katika ubora unaotakiwa na unaohitajika.
“Kampuni yetu ina zaidi ya miaka arobaini kwenye ujenzi, kwahiyo tuna uzoefu na masuala ya ujenzi tutajenga kwa ubora wa hali ya juu sana na tutajenga na kukamilisha ujenzi kwa wakati kulingana na mkataba tuliosaini” amesema Bw. Chao
