Madaktari bingwa kutoka nchi 13 kushiriki mafunzo MOI

Dar es Salaam, 18/01/2021. Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amefungua mafunzo maalum ya matibabu na upasuaji wa mgongo uliopinda (Scoliosis) kwa madaktari bingwa wa Ubongo, Mgongo na  Mifupa ambapo madaktari bingwa kutoka zaidi ya nchi 13 za Afrika mashariki, kati na kusini watashiriki.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa njia ya mtandao wa ‘zoom’ kwa siku 14 ambapo madaktari bingwa 100 wanatarajiwa  kushiriki. Mafunzo hayo yameratibiwa kwa ushirikiano kati ya MOI, hospitali ya chuo kikuu cha Weill Cornel cha Marekani pamoja na chuo cha madaktari bingwa wa upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (COSECSA).

Dkt. Boniface amesema pamoja na changamoto ya ugonjwa wa Corona unaosumbua mataifa mbalimbali duniani, Taasisi ya MOI imekuwa ikiendesha makongamano na mafunzo mbalimbali kwa  kwa lengo la kuwajengea uwezo wataaalamu wa ndani ili waendelee kutoa huduma bora kwa wa watanzania.

“Serikali ya awamu ya Tano imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu, vifaa tiba pamoja na mafunzo kwa wataalamu hapa MOI, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunawejengea uwezo wataalamu wetu kwa kuwapa mafunzo kama haya mara kwa mara ili waendane na teknolojia ya matibabu iliyopo kwenye mataifa yaliyoendelea” Alisema Dkt. Boniface

Kwa upande wake muwakilishi wa hospitali ya chuo kikuu cha Weill Cornel cha Marekani Prof.  Roger Hartl amekiri kushuhdia mageuzi makubwa yaliyofanywa Serikali ya Tanzania katika Taasisi ya MOI na kuahidi kuudumisha ushirikiano kati ya MOI na hospitali yake kwa lengo la kunufaisha pande zote mbili.

Mratibu wa mafunzo hayo Dkt. Juma Magogo amesema mafunzo yanalenga kuwapa madaktari bingwa mbinu za kisasa zaidi za matibabu ya mgongo uliopinda  kwani teknolojia ya matibabu inabadilika kila wakati hivyo ni muhimu kupata mbinu mpya mara kwa mara.

Dkt. Magogo amesema madaktari watakaoshiriki mafunzo watatoka mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi,Zimbabwe, Msumbiji, Rwanda, Burundi, Sudan, South Sudan, Ethiopia ,Namibia ambapo wakufunzi watatoka mataifa ya Marekani, Italy na Palestina.