Huduma za kibingwa za MOI kuanza kutolewa mkoani Lindi

Lindi, 19/07/2019. Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI kuanzia tarehe 1/08/2019 itaanza kutoa huduma za kibingwa za matibabu na upasuaji wa mifupa katika hospitali ya Nyangao mkoani Lindi kwa lengo kuwapunguzia wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara changamato ya kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma za mifupa.

Huduma hizi zinaanza kufuatia Taasisi ya MOI na Hospitali ya Nyangao kuingia mkataba wa ushirikiano ambapo Madaktari bingwa wa MOI watakua wanatoa huduma , upasuaji  kwa wagonjwa katika hospitali Nyangao Lindi pamoja na kuwafundisha madaktari na wauguzi.

Mkataba wa ushirikino kati ya MOI na Nyangao umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface pamoja na Daktari wa Bingwa wa Hospitali ya Nyangao Dkt Richacrd Jankiewics. Mashuhuda wakiwa Bi Prisca Tarimo Menjeja chumba cha Upasuaji MOI pamoja na Afisa utawala wa hospitali ya Nyangao Bw. Charles Laizer.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema MOI imekubali kuanzisha ushirikiano na Hospitali ya Nyangao ili kuwasogezea wananchi wa kanda ya kusini huduma kwani kwa kipindi kirefu wamekua wakisafiri umbali mrefu hadi MOI kufuata huduma za mifupa.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma zetu zinawafikia wananchi  katika ngazi zote za mikoa na wilaya hivyo wananchi wa ukanda huu wa kusini wataanza kupata huduma za mifupa hapahapa ambapo madaktari bingwa wetu watakua wanakuja hapa wanatoa huduma kwa wananchi”Alisema Dkt Boniface

Kwa uapande wake Daktari Bingwa wa Hospitali ya Nyangao Dkt Richard Jankiewics amesema wamekua wakikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa madaktari Bingwa wa mifupa katika ukanda huu wa kusini hivyo kupelekea kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda MOI kufuata huduma hizo .

“Tunaishukuru Taasisi ya MOI kwa kukubali ombi letu la kuanzisha ushirikiano ili walete wataalamu kutibu hapa, ni ukweli usiopingika kwamba ukanda huu wa kusini kuna uhaba mkubwa wa madaktari bingwa wa mifupa hivyo hatua hii italeta mageuzi makubwa kwenye huduma na naamini wananchi wengi watanufaika” Alisema Dkt Jankiewics

Taasisi ya MOI inatekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya Tano la kusogeza huduma za kingwa kwa wananchi na kuwapunguzia changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma Dar es Salaam.