Baraza la wafanyakazi MOI laazimia kuboresha huduma za kibingwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI, Dkt Respicious Boniface amefungua Kikao cha Nne cha Baraza la Nne la Wafanyakazi MOI kinachofanyika katika Ukumbi wa ‘National Carbon Monitoring Centre’ (NCMC) ulioko ndani ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.  Kikao hicho kinachofanyika kwa siku mbili  kinahudhuriwa na zaidi ya wajumbe 50 kutoka katika idara na vitengo vyote vya MOI.

Dkt. Boniface amesema katika kipindi cha miaka 5 ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Taasisi ya MOI imefanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu jambo ambalo limepekea kumaliza rufaa za kupeleka Wagonjwa nje ya nchi.

“Tumekutana hapa kwa lengo la kujadili kwa kina na kutengeneza mikakati kabambe ya kuendelea kuboresha huduma zetu.  Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vifaa tiba hapa MOI.  Sasa hivi tunavyo vifaa vya kisasa kabisa kama vile vinavyotumika katika hospitali kubwa duniani hivyo nimshukuru sana Mh. Rais kwa moyo wake wa upendo kwa Watanzania na sasa hatupeleki Wagonjwa nje ya nchi tena” Alisema Dkt. Boniface.

Pia, Dkt Boniface amewaomba Watumishi wote wa MOI wenye mawazo ya kibunifu yanayolenga kuboresha huduma au kuanzisha huduma mpya pamoja na kukuza pato la Taasisi, wayapeleke mawazo hayo ofisini kwake yatapokelewa, kufanyiwa uchambuzi na kutekelezwa.

Kwaupande wake Mwenyekiti wa TUGHE mkoa wa Pwani, Ndg. Shadrack Mkodo amewakumbusha Watumishi juu ya kufuata sheria na kanuni za Utumishi wa Umma ambazo pamoja na mambo mengine zinaweka msisitizo juu ya uwajibikaji kwa Watumishi ili kuleta matokeo bora kwa Taasisi na kwa taifa kwa ujumla.

Katibu wa Baraza la Wafanyakazi MOI, Ndg. Ngina Mitti amesema Kikao cha Baraza la wafanyakzi kitafanyika kwa siku mbili, yaani tarehe 27/08/2020 na 28/08/2020 kikiwa na Wawakilishi wa Watumishi wa MOI ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa kwa lengo la kuboresha huduma na maslahi ya Watumishi wa MOI.

Ndg. Ngina amesema kuwa vikao vya Baraza hilo la Nne limefadhiliwa na Benki ya NMB pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).